Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Kanali Aggrey John Magwaza ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kibondo ameyahimiza Mashirika yasiyo ya kiserikali kutoa huduma kwa kuzingatia misingi na maadili ya kitanzania.
Kanali Magwaza amesema hayo katika Warsha ya Mkutano wadau wa Mashirika yasiyo ya kiserikali Wilayani Kakonko iliyofanyika Mei 16, 2023, katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko.
Mkuu wa Wilaya ameeleza katika kipindi hiki yameibuka mashirika yanayounga mkono suala la ndoa za jinsia moja jambo ambalo si jema katika jamii za kiafrika, hivyo ameyasisitiza mashirika kutotekeleza shughuli hizo hata kama ni sehemu ya majukumu yao.
Aidha katika hotuba yake ameeleza anatambua mchango mkubwa unaotolewa na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na anayapongeza kwa mchango huo vile vile kuna baadhi ya mashirika yasiyokuwa ya kiserikali hapa nchini yamekuwa hayazingatii wajibu wao wa kisheria hivyo kusababisha malalamiko na manung’uniko kutoka kwa wananchi na baadhi ya wadau wa maendeleo wanaotoa fedha zao kuchangia katika juhudi za nchi kujiletea maendeleo.
‘Naiagiza Halmashauri kupitia ofisi ya maendeleo ya jamii kuhakikisha mashirika yote yasiyokuwa ya kiserikali yanatekeleza shughuli zao kulingana na usajili, malengo na vipaumbele vya taifa, aidha ninayataka mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yajielekeze kufanya kazi maeneo yenye uhitaji ikiwemo vijiji badala ya kujikita maeneo ya mjini pekee’. Alisema kanali Aggrey Magwaza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko Ndaki Stephano Mhuli ameeleza mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yamekuwa na msaada mkubwa sana katika Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko kwani mashirika yanafanya kazi nzuri ya kuchangia katika ujenzi wa madarasa, ujenzi wa vituo vya afya, ujenzi wa wodi ya mama na mtoto pia wamefanya shughuli ya ugawaji wa taulo kwa watoto wa kike shuleni na ugawaji wa baiskeli kwa wanafunzi wa kike wanaotembea umbali mrefu hasa wanaoishi katika mazingira magumu.
CHANZO:HALMASHAURI WILAYA KAKONKO
Comments
Post a Comment