Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Kakonko Col.Aggrey Magwaza amefanya kikao cha kwanza cha Kamati ya maandalizi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 na kupitisha miradi itakayopitiwa na kutembelewa na Mwenge wa Uhuru utakaokimbizwa Wilayani Kakonko tarehe 16 Agosti, 2023.
Col. Aggrey Magwaza ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kibondo anayekaimu nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Kakonko amekutana na wajumbe wa kamati ya Maandalizi ya mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko leo Mei 17, 2023.
Miradi iliyopendekezwa na kupitishwa kutembelewa na Mwenge wa Uhuru 2023 ni Uzinduzi wa vyumba 08 vya madarasa na ofisi 3 za waalimu shule ya Sekondari ya wasichana Kakonko, Kutembelea kikundi cha Vijana bodaboda Muganza, Uzinduzi wa kiwanda cha kutengeneza mkaa mbadala kikundi cha Vijana Itumbiko, Kuweka jiwe la Msingi nyumba ya Mkuu wa Wilaya (Ikulu ndogo Kakonko) inayojengwa Itumbiko, Kukagua Barabara ya lami Kakonko-Itumbiko inayoelekea hospitali ya Wilaya, Kutembelea sheli ya mafuta ya “Glory to God” iliyopo karibu na stendi kuu ya mabasi, Kutembelea klabu ya wapinga Rushwa na Madawa ya kulevya Buyungu sekondari, Uzinduzi wa Ofisi ya Afisa Tarafa Kasanda na Ufunguzi wa wodi tatu za Hospitali ya Wilaya ya Kakonko.
Col. Aggrey Magwaza amewasisitiza wajumbe kufanya kazi kwa kushirikiana kama timu kwani itasaidia Wilaya ya Kakonko kufanya vizuri katika mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 na miradi kuleta tija kwa Wananchi kutokana na kuzingatia ubora wakati wa ukamilishaji wake.
Kauli Mbiu ya mwaka huu, “Tunza Mazingira, okoa vyanzo vya maji kwa ustawi wa viumbe hai na Uchumi wa Taifa.”
Wilaya ya Kakonko itapokea Mwenge wa Uhuru kimkoa tarehe 16 Agosti, 2023 kutokea Wilaya ya Biharamulo iliyopo mkoa wa Kagera.
CHANZO:Kakonko Dc
Comments
Post a Comment