Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
ameagiza Wizara za Serikali zinahusika na kodi na mawasiliano pamoja na
makampuni ya simu za mikononi nchini kukutana mara moja kutafuta jinsi
gani ya kumaliza mvutano wa kodi mpya ya kadi za simu hizo za mikononi.
Rais kikwete ametoa maelekezo hayo jioni ya leo, Jumanne, Julai 23,
2013 wakati alipokutana na viongozi wa Wizara ya Fedha, Wizara ya
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na wawakilishi wa makampuni ya simu
ya TTCL, Airtel, Vodacom, Tigo na Zantel katika kikao cha pamoja
kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
Rais Kikwete amesema kuwa lengo kuu la mkutano huo wa pamoja kati ya
Wizara hizo za Serikali na makampuni ya simu yawe ya kupendekeza jinsi
gani ya kuziba pengo la Sh. Bilioni 178 ambazo zitapotea katika Bajeti
iwapo kodi hiyo kwa kadi za kuongelea za simu za mikononi italazimika
kufutwa na Serikali kupitia marekebisho kwenye Muswada wa Fedha wa
Bajeti ya Mwaka 2013/2014.
Rais Kikwete amewaambia wawakilishi
wa pande hizo mbili kuwa huwezi tena kuifuta moja kwa moja kodi hiyo
bila kutafuta njia nyingine za kupata fedha za kujaza pengo hilo la Sh.
Bilioni 178 ambazo tayari Bunge limezipangia matumizi.
“Nawaombeni
kaeni pamoja, wekeni bongo zenu pamoja, wekeni akili yenu pamoja
tutafute namna gani tunaweza kujaza pengo hili la Sh. Bilioni 178 endapo
tutakubaliana kuwa kodi hii inawabebesha wananchi mzigo mzito na kuwa
pengine menejimenti ya kodi yenyewe ni ngumu,” Rais Kikwete amewaambia
wawakilisho hao.
Katika Bajeti ya Serikali ya mwaka 2013/2014,
Serikali imeweka kodi ya Sh. 1,000/= kwa mwezi kwa kila mtumiaji simu
kwa ajili ya kufanya mawasiliano kwa kutumia simu ya mkononi.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
23 Julai, 2013
- Get link
- X
- Other Apps
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment