Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amejipeleka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi ikiwa ni siku moja baada ya kundi la polisi wenye silaha za moto kuvamia nyumbani kwake kwa nia ya kumkamata.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, jana alisema Mbowe, ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, aliripoti Makao Makuu ya Jeshi hilo jana saa 8:45 mchana na kuhojiwa na polisi kwa zaidi ya saa tano.
Msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso, alithibitisha Mbowe kuripoti Makao Makuu ya Polisi kwa ajili ya kuhojiwa.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Mnyika, ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo (Chadema), Mbowe aliachiwa jana saa 1:45 usiku baada ya kudhaminiwa naye (Mnyika) na kwamba, ametakiwa kuripoti tena Julai 23, mwaka huu, saa 8 mchana.
Mnyika alisema Mbowe alihojiwa kwa tuhuma za uchochezi unaodaiwa kuwa unatokana na tamko alilolitoa baada ya Kamati Kuu ya Chadema kuhusisha polisi na mlipuko wa bomu uliotokea jijini Arusha.
Mlipuko huo ulitokea katika mkutano wa hadhara wa kufunga kampeni za chama hicho kwa ajili ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata nne za jiji hilo Juni 15 mwaka huu.
Alisema tuhuma nyingine ni madai yake kuwa polisi walipanga kukisaidia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi wa Arusha na Rais Jakaya Kikwete na serikali kutoshiriki katika mazishi kwamba, ni ishara ya hisia za hatia kwa kuwa anatambua njama zinazopangwa na polisi dhidi ya Chadema.
Kwa mujibu wa Mnyika, katika mahojiano hayo, Mbowe alikuwa na mawakili; Peter Kibatala na Nyaronyo Kicheere.
Alisema viongozi waliomsindikiza ni pamoja na yeye (Mnyika), Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo, Benson Kigaila na Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri wa Chadema, John Mrema.
“Tutaeleza yaliyojiri baada ya mahojiano kukamilika,” alisema Mnyika.
Juzi kundi la polisi wenye silaha za moto walivamia nyumbani kwa Mbowe, kwa nia ya kumkamata.
Kwa mujibu wa gazeti moja litokalo kila siku (siyo NIPASHE), askari hao wanaokadiriwa kufikia saba, wakiwa na silaha nzito katika gari la wazi waliwasili nyumbani kwa Mbowe majira ya saa 7:30 na kuwaamuru askari wanaolinda nyumbani kwake kumtoa Mbowe nje ili waonane naye.
Walinzi wa Mbowe walihoji uhalali wa ukamataji huo na kuwataka polisi wawaonyeshe hati ya kumkamata, lakini hawakuweza kuionyesha, hali iliyozusha wasiwasi kwa walinzi wa kiongozi huyo.
Hata hivyo, walinzi hao waliwaambia polisi hao kuwa Mbowe alikuwa safarini.
Polisi hao baada ya kuona wameshindwa kukamilisha kazi hiyo, waliwaachia walinzi hao namba ya simu ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Ernest Kimola, wakiwaagiza kuhakikisha wanamwambia Mbowe awasiliane na kamanda huyo.
Akizungumza na NIPASHE jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alisema hawezi kuzungumza lolote kuhusiana na suala hilo kwa kuwa haliko ndani ya eneo la mipaka ya kazi yake.
Hata hivyo, alisema hakuna muda maalum uliowekwa na sheria kumkamata mtuhumiwa.
CHANZO: NIPASHE
Comments
Post a Comment